SIKU YA MTOTO WA AFRIKA DUNIANI IWE SIKU YA KUMKOMBOA MTOTO WA MTAANI TANZANIA
Siku ya mtoto wa Afrika ni sikukuu ambayo hufanyika kila mwaka duniani ikiwa na lengo la kuenzi na kuimarisha maisha ya watoto duniani.
Siku hii huwa na lengo la kupafanya duniani kama mahala salama kwa watoto, wakati dunia ikichagua kusherehekea kila tarehe kumi na sita Juni, sikukuu hii ya mtoto wa Afrika duniani.
Huwa nafarijika kuona jinsi gani dunia imeamua kuthamini na kutambua umuhimu wa watoto hapa duiani naenda mbali zaidi kifikra napoona dunia,
imemchagua mtoto wa Afrika kuwakilisha watoto wengine duniani, katika siku kama hiyo yenye umuhimu mkubwa kwa watoto.
Dunia imeenda mbali zaidi tena kwa kuchagua sikukuu hii itambulike kama siku ya mtoto wa Afrika, mtoto kutoka bara masikini lenye nchi nyingi za ilimwengu wa tatu.
Wakati haya yote tukijivunia Afrika imeendelea kushika rekodi kwa kuwa na matukio mengi ya kikatili dhidi ya watoto ukatili wa kijinsia na ajira kwa watoto.
Wakati mwingine watoto wamekuwa wakitumiwa kama wapiganaji jeshini ni rahisi sana kuona majeshi ya upinzani nchini Somalia wakiwa na wanajeshi watoto,
lakini wakati hayo yakiendelea duniani na Afrika kwa ujumla Tanzania imejikuta ikitumbukia kwenye dimbwi la kuwa moja ya nchi zinazoshika kasi ya kuwa na watoto wengi wa mitaani.
Lakini kama hiyo haitoshi Tanzani ni miongoni mwa nchi nyingi za Afrika zenye matukio ya kutisha tena ya kikatili dhidi ya watoto,
ikiambatana na mauaji ya Albino ambayo kimsingi waathirika wakubwa walikuwa watoto, lakini hebu tuwaangalie watoto wa mitaani nchini Tanzania.
Wakati ulimwengu mzima ukisherehekea sikukuu hiyo ya mtoto wa Afrika duniani, huwa najiuliza je watoto wanapewa kipaumbele katika sikukuu yao hiyo .
Kwa nchi kama Tanzania je watoto wana maisha bora ni kweli dunia au Tanzania ni mahala salama kwao kuishi, haya yote ni maswali ambayo watu wengi hujiuliza kila siku,
haswa wanapowaona watoto wa mitaani wakizagaa hovyo katika mitaa ya posta na kariakoo jijini Dar-es-salaam na katika miji mingine mikubwa ya Tanzania,
kama Mwanza na Arusha wakiwa hawana shughuli maalumu ya kufanya lakini je mtoto ni nani. Mtoto ni mtu aliye chini ya umri wa miaka kumi na nane.
Anayetafsiriwa kama kiumbe tegemezi asiyeweza kujihudumia mahitaji muhimu ya kimaisha kama chakula, nguo na maradhi.
Achilia mbali mahitaji hayo hata msaada wa kisaikolojia ni muhimu kwa mtoto, mtoto ni mtu anaye hitaji malezi na msaada wa hali ya juu kutoka kwa watu wazima walio mzidi kiumri,
kimsingi mtoto anahitaji msaada wa kibusara zaidi ya kuzidiwa umri tu,kwa watoto wa mitaani ni watoto wasio na makazi maalumu,
ambao mara nyingi huzurura na kuransa randa mitaani bila kuwa na shughuli maalumu, wakiwa hawana uangalizi wengi wa watoto hawa hutumia muda wao mwingi kutembea hovyo katika miji mikubwa.
Wakiwa hawana mwelekeo shughuli yao kubwa ikiwa kuomba fedha kutoka kwa wapita njia, huku wengine wakijishughulisha na shughuli mbalimbali kwa kufanya vibarua vidogo vidogo,
kama kuosha magari barabarani, ukipita mijini na kuwaona watoto hawa utajiuliza maswali mengi kwamba kwanini wasiwepo nyumbani au shuleni maana wengi hurandaranda mitaani bila sababu za msingi.
Zipo sababu mbalimbali zinazo fanya watoto hawa wanaonekana mijini wakizurura muda ambao ilibidi pengine wawepo nyumbani au darasani,
hasa katika kipindi kama hiki ambacho serikali imewekeza mamilioni ya fedha na nguvu za wazazi katika kuhakikisha watoto wote wanapata elimu .
Wakati haya yote yakiboreshwa kwa ajili ya watoto, kasi ya watoto wa mitaani imeendelea kukua siku hadi siku nchini Tanzania,
mfano ni jambo la kawaida ukiwa unatembea jijini Dae-es-salaam katika mitaa ya Posta, Kariakoo , Mwenge, Ubungo na maeneo ya Kawe kukutana na watoto wakiwa wachafu ,
wamepigwa na jua midomo imewakauka wakiomba pesa kutoka kwa wapita njia , wakati mwingine unaweza kuwakuta wakiwa wamelala kwenye mitaro ya maji machafu,
wengi wakiwa hawana hata nguo nzuri kusitiri miili yao, lakini kwanini watoto hawa wanazagaa mitaani, wengi wa watoto hawa hapa jijini Dar-es-salaam wanatoka mikoani
na asilimia kubwa ya watoto hawa wamewaacha wazazi wao nyumbani na kukimbilia kwenye hii miji mikubwa, wakiamini huku ndiko kwenye mafanikio makubwa kimaisha ,
Saidi Abdallah mtoto wa miaka kumi na tatu akiwa anaishi ubungo maji na shughuli zake akifanyia posta, akiwa mwosha magari.
Ananiambia alikimbia nyumbani baada ya kuona unyanyasaji kutoka kwa baba yake wa kambo umekuwa mkubwa, hivyo akatafuta nauli na kupata kutoka kwa mjomba wake,
ambaye ndiye aliyempandisha basi nakuja BONGO yani Dar-Es-Salaam, kama ambavyo wenyewe wanapaita Abdallah, anadai wakati anakuja jijini Dar-es-salaam,
hakujua anakuja kuishi vipi alichoamini yeye ni kwamba kuwa mbali na baba yake wa kambo kungempunguzia maumivu na kumpa muda wa kujipanga kimaisha,
kabla ya kurudi nyumbani kumsaidia mama yake ambaye amemkumbuka sana kwani wakati anatoroka nyumbani hakupata muda wa kumuaga ,
Salumu au Manyoni kama kijiweni wanavyo mtambua anaeleza kwa uchungu jinsi mama yake alivyoshindwa kuendesha familia na kujikuta yeye kama mtoto wa kwanza,
akilazimika kuja mjini kutafuta maisha Salumu anasema hutuma pesa nyumbani kila mwisho wa mwezi, mkoani Shinyaga wilayani Kahama akigoma ,
kutaja kijiji chake kwa hofu ya ndugu zake kuja kumtafuta , hawa ni watoto ambao safari zao za kutoka mkoani zilikuwa za kwenye mabasi wakiwa wamesimama kwa msaada wa madereva na makondakta,
lakini wengine hudandia magari makubwa ya mizigo maarufu kama malori, Kitale anasema yeye alipanda lori la kusafirishia ng’ombe kutoka Mbeya hadi jijini Dar-es-salaam mwaka 2010 wakati huo akiwa na miaka 13,
sababu kubwa iliyomfanya kuja Dar ni kwamba, aliambiwa na rafiki yake aliyekuwa jijini kwamba huku maisha ni rahisi mno,
nilipojaribu kumuuliza kuhusu huyo rafiki yake ananijibu kwa uchungu, kwamba tangu aje jijini hakuwahi kumuona.Lakini wapo watoto ambao wao hawatoki mikoani,
bali hapahapa jijini wao pia hurandaranda mijini wengine hutoroka shule na kuja mijini kuomba pesa, wengine hawasomi japo umri wao unawataka wawepo darasani .
Nilizungumza na baadhi ya watoto wakadai wazazi wao wamewaagiza kuomba pesa, wao wako nyumbani wakihudumia wadogo zao,
wakati nikifanya mahojiano na Hamisi Mnyama kama alivyojitambulisha maeneo ya mwenge nilipata bahati ya kuzungumza na wakina mama,
ambao nao walikuwa na watoto wao migongoni, wakiomba pesa kutoka kwa wapita njia na wakati mwingine watoto hawa hukaa mpaka katikati ya barabara wakiomba msaada kutoka kwa wasafiri .
Wengi wa wakina mama hawa huongozana na watoto wao wakubwa wakigawana majukumu ya kubeba mtoto mchanga mgongoni,
ukiwauliza wanawake hawa wengi wanadai wameachwa na waume zao, na wengi wao hawana uwezo wa kujitegemea na imewaladhimu kuja barabarani na kuomba msaadaili waweze kupata chakula.
Wengine wanakubali madai dhidi yao kutoka kwa watoto wao, kwamba kweli wakati mwingine huladhimika kuwatuma watoto wao kutafuta pesa, na wao kubaki nyumbani wakiwahudumia wadogo zao.
Nilipowauliza kwanini wasiwapeleke watoto wao shule, wakadai hawana hata uwezo wa kununua chakula itakuwaje kwa mahitaji ya shule.
Nilipowauliza kama wamewashitaki wanaume zao mahala husika, wengi walidai hawaja fanya hivyo hapa niligundua wengi wa wanawake hawa hawajui haki zao za msingi,
hivyo wizara ya kina mama jinsia na watoto ina jukumu la kuhakikisha kwamba wanawake wote wanajua haki zao
Kwa tathmini ya haraka utagundua tatizo la watoto wa mtaani, limekuwa kwa kiasi kikubwa likichangiwa na migogoro ya kifamilia.
Ambayo inapelekea kuvunjika kwa ndoa au familia nyingi na hivyo kupelekea watoto kukimbia nyumbani, wengi wakitoka maeneo ya kaskazini, kusini na maeneo ya kati,
ya nchi yetu nzuri yenye rasilimali za kutosheleza lakini ikiwa bado moja ya nchi masikini, zilizoshindwa hata kusimamia sera na ahki za mtoto,
nawaza sana juu ya juhudi za baba wa taifa hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, aliyekuwa na ndoto za kuona kila mtoto anapata malezi na kuwa na maisha bora.
Lakini leo watoto wamekuwa waathirika wakubwa wa madawa ya kulevya wamekuwa walevi wa pombe ,sigara na wengine wakijihusisha na ngono katika umri mdogo.
Watoto wamekuwa wakihusishwa na matukio ya kikatili , unyanyaswaji wa kijinsia na wengine wakiuawa kwa vipigo vikali kutoka kwa wazazi au ndugu baki wa karibu,
matatizo haya yamekuwa yakiambatana na ajira kwa watoto, hasa kazi za ndani na kufanyishwa biashara za ngono kwenye madanguro hasa watoto wa kike,
wanaowekwa kwenye hatari ya kuambukizwa magonjwa hatari kama ukimwi. Nafahamu sio kila mtoto anaishi mtaani kutokana na sababu nilizotaja hapo juu,
wengine hulka ya kujaribu vitu vipya na misukumo hasi kutoka kwa marafiki, inapelekea watoto hawa kuacha misingi imara waliyo lelewa na kutoka nje ya mstari au maadili mema,mwisho hutoroka nyumbani na kuingia mtaani.
Juhudi zinafanywa na serikali katika kuwakomboa watoto hawa, lakini bado sijaridhishwa na utendaji wa viongozi wa wizara husika,
wenye mamlaka ya kutunga na kusimamia utekelezwaji wa sera na haki zinazo mlinda motto, bado wako nyuma katika kutekeleza haki hizo ikiwemo elimu ,chakula na maradhi hivi ni vitu ambavyo dunia imehalalisha,
kwamba kila mtoto anapaswa kuwa navyo kwa gharama yoyote, kwa vyovyote vile serikali itumie muda huu wa kujadili katiba mpya, kupitia upya haki za watoto na kuunda sera mpya,
zitakazo mlinda mtoto na pia watoto wapewe kipaumbele cha kusikilizwa, wafahamishwe juu ya kasoro zao na sio kufukuzwa nyumbani pale inapoonekana wana mapungufu Fulani.
Ni wakati sasa wa kuchagua malezi bora kwa kila mtoto na sio bora malezi,ni wakati sasa wa kuhakikisha tunawapa watoto wetu wote wa Tanzania familia bora.
Hebu tafakari kama serikali ingejenga vituo kumi kila mkoa kwa ajili ya watoto hawa wasio na makazi maalumu , nchi hii inayoshutumiwa na wananchi kutumia mali asili zake vibaya ingekuwa wapi.
Watanzania tuna miezi takribani mitano mbele yetu kabla ya kuifikia sikukuu ya mtoto wa Afrika, hebu tutumie muda huu kujiandaa na ukombozi wa mtoto wa mtaani Tanzania.
Siku hiyo kila Mtanzania atabeba bango kwa ajili ya ujumbe kwa watoto wa mitaani, kwamba wao nao wana haki kama watoto wengine waliopo majumbani.
Na pia tusahau yaliyopita yakatuumiza ni wakati wa kukumbuka tulipokwama, katika juhudi za kumkomboa mtoto wa mtaani wa Tanzania.
Ili na yeye siku moja aone fahari kuitwa mtoto wa Afrika, tukumbuke kila mtoto ni mtoto wa mtaani mtarajiwa kwani hata hao wa mtaani hawakuwahi kutarajia kuwa hapo walipo sasa.
Tuwapende, tuwabebe na tuwalinde wanatuhitaji, amani kwa watanzania wote nawatakia heri ya mwaka mpya wenye nguvu na amani tusisahau kumuomba mungu amen